Zitto Kabwe asema,Waziri Mkulo akae pembeni apishe Uchunguzi Zaidi

By Gadiola Emanuel - 2:40:00 PM

  
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Fedha ndugu Mustafa Mkulo akae pembeni kupisha uchunguzi dhidi yake kuhusu Shirika la CHC.

Katika Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi kulitokea malumbano makali kati ya  Serikali na Wabunge wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma kuhusu kuongezwa muda wa Shirika la CHC. Wakati Waziri wa Fedha alileta Azimio la kulivunja Shirika hili lenye taarifa nyingi na nyeti kuhusu zoezi la Ubinafsishaji, Kamati ya Bunge ya POAC kutokana na uzoefu wake wa kukagua mahesabu ya Mashirika ya Umma na kufuatilia zoezi la Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma, ilipinga hatua hii na kulitaka Bunge kukataa Azimio la Serikali na kulifanyia marekebisho makubwa. Hatimaye Bunge liliridhia kufanya mabadiliko makubwa katika Azimio la CHC, kwa kuamuru Shirika lipewe uhai wa miaka 3 na kuagiza uchunguzi wa namna bora ya kuendesha shughuli za Shirika la Consolidated Holdings. Mapendekezo ya Kamati ya POAC ni kulifanya Shirika hili kuwa la kudumu na kulipa jukumu la kumiliki na kusimamia uwekezaji wa Serikali kwenye kampuni binafsi (National Investment Agency) kama ilivyo Shirika la Tamasek ya Singapore na Shirika la Khazana ya Malaysia. Kwa sasa Uwekezaji wa Serikali katika Kampuni binafsi unasimamiwa na Hazina na usimamizi wake ni mbovu na hauleti tija kwa Taifa.
Kitendo cha kushindwa kwa hoja Bungeni kiliifedhesha Serikali na hivyo kwa kupitia Wizara ya Fedha kuamua kulihujumu Shirika kwa kumsimamisha Mkurugenzi wake Mkuu kwa makosa ya kimajungumajungu na kwa kuzusha kwamba CHC iliwahonga wabunge ili kuitetea.  Waziri wa Fedha ndugu Mustafa Mkulo alilitaarifu Bunge kuwa Bodi ya CHC imeomba ukaguzi maalumu kuhusu tuhuma za ubadhirifu ndani ya Shirika hilo. Niliitaka Serikali ichunguze pia tuhuma kwamba Kamati ya POAC ilihongwa na kuahidi kuahidi kujiuzulu nyadhifa zangu zote ikithibitika.
Katika Uchunguzi wake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Heabu za Serikali kwa kupitia Kampuni ya Ernest and Young walitaka kufanya mahojiano na Waziri wa Fedha juu ya tuhuma mbalimbali zinazomkabili ndani ya CHC. Waziri Mkulo alikataa kuhojiwa na wakaguzi na badala yake akaandika barua (kumb TYC/B/70/2/03 ya Oktoba 8, 2011) yenye kujibu tuhuma moja, tena kwa juu juu, kuhusu yeye kuliamuru Shirika kuuza kiwanja cha Shirika bila kufuata taratibu za sheria. Wakati Waziri anakanusha kuliagiza Shirika kuuza kiwanja kwa mtu aliyemtaka yeye, mimi nina ushahidi tosha wa Nyaraka kutoka Hazina, kwa mfano barua TYC/A/290/13/4 ya Machi 9, 2011 ambayo inawagiza CHC kutekeleza agizo la Waziri la Fedha kuhusu kiwanja na. 10 barabara ya Nyerere. Vilevile, nina ushahidi wa mkutano uliofanyika huko Morogoro Hotel kati ya Waziri wa Fedha na Mwenyekiti wa Bodi ya CHC kuhusu jambo hilo.
Siku mbili baada ya kumjibu CAG, Waziri wa Fedha ndugu Mustafa Mkulo aliamua kutengua uamuzi wake wa kuongeza muda wa Bodi ya Shirika la CHC mpaka mwezi Disemba 2011 na hivyo kuivunja. Uamuzi huu wa Waziri una lengo la kuficha ukweli kwani CHC bila Bodi ya Wakurugenzi inaendeshwa na Hazina na hivyo taarifa ya ukaguzi itabidi ipelekwe Hazina ambayo Waziri wake ni mtuhumiwa.
Uchunguzi wa kina
Ninapendekeza uchunguzi wa kina ufanyike kwa kutumia vyombo vya dola na hasa TAKUKURU kuhusu tuhuma hizi dhidi ya Waziri wa Fedha na alazimishwe  kisheria kujibu maswali ya wakaguzi (Auditors) kuhusu tuhuma dhidi yake.
Wakati uchunguzi unaendelea ndugu Mustafa Mkulo asimamishwe kazi ya Uwaziri wa Fedha hadi hapo uchunguzi utakapokamilika. Kitendo chake cha kuiamuru Bodi kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu kwa tuhuma za kutunga na majungu na baadaye kuvunja Bodi ya CHC wakati inasubiri taarifa ya uchunguzi kutoka kwa CAG ni kuingilia uchunguzi na pia ni matumizi mabaya ya Ofisi ya Umma ili kulinda maslahi binafsi. Ni dhahiri akiendelea kuwa Waziri wa Fedha ataharibu uchunguzi.
Vilevile, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Jakaya Kikwete aangalie kama anaitendea haki nchi na Uchumi wa nchi kwa kuwa na Waziri wa Fedha ambaye anasema uwongo Bungeni bila kuogopa na mwenye kutumia Ofisi yake vibaya kwa kuchukua maamuzi yanayoingilia uchunguzi unaomhusu ili kujilinda.
Taarifa ya Uchunguzi ikabidhiwe kwa Spika
Kutokana na ukweli kwamba suala la CHC lilianzia Bungeni na hata Waziri mwenyewe kukiri kuwa taarifa ya uchunguzi inapaswa kuwekwa wazi. Kutokana na matokeo ya sasa ambapo Waziri wa Fedha mwenyewe ana tuhuma za kujibu na kwamba hivi sasa hakuna Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika na hata itakayoundwa itateuliwa na Waziri mtuhumiwa ninashauri kuwa taarifa ya uchunguzi wa Shirika la CHC sasa ipelekwe kwa Spika wa Bunge kwa hatua zaidi.

Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi

  • Share:

You Might Also Like

0 comments