Kenya yaanza mapigano ndani ya Somalia

By Gadiola Emanuel - 6:32:00 AM

Vikosi vya Kenya
Vikosi vya Kenya

Vikosi vya Kenya vimepambana na wanamgambo wa kiislamu wa al-Shabab ndani ya Somalia kwa mara ya kwanza tangu kuvuka mpaka na kuingia nchini humo wiki mbili zilizopita.
Msemaji wa jeshi la Kenya Major Emmanuel Chirchir ameiambia BBC kuwa msafara ulishambuliwa kati ya miji ya Tabda na Bilis Qoqani.
Kila upande umesema mwenzake alishambuliwa.
Major Chirchir alisema kuwa wapiganaji tisa wa al-Shabab waliuawa na wanajeshi wawili kujeruhiwa, mmoja vibaya sana.
Al-Shabab kwa upande wake unakanusha idadi hiyo na kusema kuwa wakenya 20 ndio wameuawa na msemaji wa kundi hilo Abdul Asis Abu Muscab, amewaambia waandishi kuwa huu ndio mwanzo tu wa mapigano na mashambulizi zaidi yatafuatia.
Wakazi katika eneo hilo wanasema kuwa makabiliano yaliohusisha pia ufyatulianaji risasi yalidumu kwa nusu saa.
Kenya iliwatuma wanajeshi wake kusini mwa Somalia mapema mwezi huu, ikishutumu kundi la al-Shabab kwa msururu wa utekaji nyara Kenya.
Al-Shabab, kundi linalodhibiti eneo la kati na kusini mwa Somalia limekuwa likikanusha madai hayo na limetishia kuishambulia Kenya kulipiza kisasi.

Marekani yajiandaa kwa mashambulizi


Wakati huohuo Marekani imeanza kufanyia majaribio ndege zake za kivita zisizo na rubani nchini Ethiopia katika maandalizi ya kuanza mashambulio dhidi ya ngome za wapiganaji wa Al Shabaab Somalia.

Ndege hizo ambazo zinaweza kubeba makombora na mabomu yanayoelekezwa kwa kutumia mtambo wa satelite zitaruka kutoka kituo cha jeshi la Marekani katika mji wa kusini mwa Ethiopia wa Arba Minch.
Marekani hatahivyo imeihakikishia serikali ya Ethiopia kwamba ndege hizo hazina silaha kwa hivi sasa na zinatumika tu kuchunguza hali ya usalama.
Marekani imekuwa ikitumia ndege hizi nchini Djibouti ambako majeshi yake yana kambi yake ya kijeshi ikiwa ndio kambi ya kipekee ya majeshi ya Marekani barani Afrika.
Hayo yakiendelea Mkenya mmoja ambaye amekiri kuwa mwanachama wa al-Shabab, amehukumiwa kifungo cha maisha baada ya kukiri kuhusika na mashambulizi mawili ya gurunti katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.

Mwandishi wa BBC Noel Mwakugu akiwa mahakamani amesema kuwa Elgiva Bwire Oliacha alionekana kutabasamu wakati akipigwa picha na kusema kuwa hajuti kwa kile alichokifanya na kuwa hatakata rufaa kupinga hukumu yake.
Mtu mmoja aliuawa na wengine 29 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo mawili katika kilabu kimoja na kituo cha basi.

  • Share:

You Might Also Like

0 comments