Mwanariadha Sarah Ramadhan ahujumiwa katika mbio za Muungano Marathon

By Gadiola Emanuel - 8:44:00 AM



Na Clezencia Tryphone
................................................
MRATIBU wa mbio za Muungano Marathon zilizodhaminiwa na Kampuni ya Home Shopping Center, Sara Ramadhan, amewalaumu baadhi ya viongozi wa juu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), kwamba wamehujumu mbio hizo zilizofanyika juzi, jijini Dar es Salaam na nyingine alizowahi kuziandaa.
Sara, mwanariadha wa zamani aliyekuwa akishiriki mchezo wa mitupo, miluko, tufe na kisahani, amekuwa akiratibu mbio mbalimbali kwa lengo la kukuza mchezo huo, lakini amedai amekuwa akifanyiwa hila na baadhi ya viongozi.
Mbali ya mbio hizo za Muungano zilizofanyika kwa mara ya pili mwaka huu, Sarah pia amekuwa akiratibu mbio ambazo hufanyika kila Mkesha wa Mwaka Mpya ‘New Year Eve Midnight Marathon.’
Sarah aliyeratibu matukio hayo kupitia Klabu yake ya Nyro Athletics, alisema jana kuwa baadhi ya viongozi wa RT wamehusika kuhujumu mbio zake za Jumapili kwa kuwapoteza washiriki, hivyo kushindwa kufuata njia kama ilivyopangwa.
“Sijui kwa nini viongozi wa juu wa RT, wananihujumu mbio zangu sio hizi tu (Muungano), hata za mkesha wa mwaka mpya walifanya hivyo kwa kuiba bango la kuanzia mbio ambalo lilikuwa na nembo ya mdhamini Kampuni ya Mohamed Enterprises, kwa nini wananifanyia hivi wakati wao hata kuanzisha mbio hawawezi? Naamini watashindwa tu,” alisema Sara bila kuwataja wahusika moja kwa moja.
Sara alisema katika mbio za juzi, viongozi hao hao ambao hakupenda kuwataja, walimpoteza polisi aliyekuwa anaongoza msafara, kuwapitisha vituo washiriki na kuhoji kama Tanzania inahitaji mchezo huo kupiga hatua watu wenye roho hizo wakae kando.
Katika mbio hizo za juzi, Watanzania waliongoza kwa upande wa wanaume. Washiriki walishindana katika mita 100, 400, 800, 1500, 3000, 5000 na 10,000.
Aidha kulikuwa na mitupo ambapo washiriki walitupa kisahani na tufe pamoja na kuruka vihunzi mita 100.
Hata hivyo, Sarah ametoa shukrani kwa kampuni ya Home Shopping Centre kwa udhamini wao uliofanikisha mbio hizo ingawa aliwafuata siku chache kabla ya kuanza tukio hilo.
Juhudi za kuwapata viongozi wa RT kuzungumzia madai ya Sarah, hazikufanikiwa kwa siku ya jana hadi tunakwenda mitamboni.

  • Share:

You Might Also Like

0 comments