HOTUBA YA IGP KUHUSU MPANGO WA KUWAJENGEA UWEZO VIONGOZI WA DINI KUHUSU MIUNDOMBINU YA AMANI

By Gadiola Emanuel - 2:56:00 PM

NDUGU ZANGU VIONGOZI WA DINI, WAANDISHI WA HABARI, ITIFAKI IMEZINGATIWA.

1. Awali ya yote napenda niwashukuru kwa kuitikia wito wangu na kukubali kuacha kazi zenu zingine za kulitumikia Taifa, ili hatimae tuweze kukaa pamoja na kubadilishana mawazo tukilenga jambo muhimu, ambalo ni umuhimu wa Jamii yetu kuwa na Utii wa Sheria bila Shuruti.

2. Uhuru wa kuabudu unabainishwa, kutambuliwa na kulindwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu. Uhuru huu wa kuabudu ili uweze kuendelea kuwa chachu ya upendo, umoja, maelewano na amani katika nchi yetu, Jeshi la Polisi linalenga kushirikiana na nyinyi viongozi wa dini, ili kuweza kutambua na kubainisha mamlaka zilizopo na wajibu wa jamii katika kujenga na kudumisha miundombinu ya amani na fursa waliyonayo katika kuzuia na kupambana na uhalifu katika jamii husika, hasa kwa kuwa chachu ya ujenzi wa jamii adilifu na yenye tabia ya utii bila shuruti.

3. Wajibu wa Madhehebu ya Dini, Ndugu zangu, katika nchi yetu yapo madhehebu mbali mbali ya dini, lakini yote yanatawaliwa na kusimamiwa na maelekezo yaliyoainishwa kwenye ibara ya 19 ya katiba ya nchi yetu. Mbele ya sheria hakuna dini iliyo bora kuliko dini nyingine. Dini zote zina uzito sawa mbele ya sheria. Kwa mujibu wa sheria, madhehebu yote yana wajibu ufuatao kwa masilahi ya jamii:-
kudumisha Usalama wa Jamii, Amani katika jamii, kulinda maadili ya jamii na kujenga Umoja wa Taifa letu. Aidha, dini ni sehemu ya utamaduni wa jamii na kwa tafsiri iliyopana dini zinapaswa kuwa ni gundi au sementi inayoshikamanisha jamii na kuipa ufahamu wa kutambua na kuthamini maadili ya jamii, umoja na mshikamano wa Taifa.

4. Miongozo ya dini, utawala na kuithibiti dhamira za wafuasi, ambamo ndimo liliko chimbuko la mema au matendo ya kihalifu, ndiyo sababu kubwa inayofanya tukutane hapa leo, kwamba, madhehebu ya dini yana dhamana kubwa ya kusimamia dhamira za watu, katika ujenzi wa jamii adilifu na kuepusha vurugu au matendo mengine yanayoweza kuathiri maendeleo ya jamii na ustawi wa Taifa letu.

5. Lengo la kikao hiki ni utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyotangulia baina ya viongozi wa dini na Jeshi la Polisi, ambayo yalilenga mkakati wa kudumisha amani, usalama na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Vilevile, ni muda mwafaka wa kujipanga kwa pamoja katika kuihimiza jamii juu ya Utii wa Sheria bila Shuruti na urejeshaji wa umoja na mshikamano wa dhati katika jamii ulioathiriwa kwa namna moja au nyingine na kampeni za kuwania uongozi katika uchaguzi mkuu wa 2010. Hata hivyo, nyinyi viongozi wa dini kwa kutambua wajibu wenu na mnavyowajibika katika ujenzi wa jamii adilifu mna nafasi kubwa ya kuhimiza wafuasi wenu kutii sheria za nchi bila shuruti.

6. Mwisho naomba nimalizie kwa kuwashukuru tena kwa kukubali wito wangu, nikiamini yale yote tutakayokumbushana na kuyajadili hapa yatakuwa ni chachu katika kuimarisha hali ya amani, usalama na utulivu kwa kutoa elimu kwa wengine walio chini yetu namna ya kuwa na utii wa sheria bila shuruti. Na hii ndiyo dhana nzima ya utekelezaji wa ulinzi shirikishi kwa vitendo. AHSANTENI SANA.

  • Share:

You Might Also Like

0 comments