Ghasia zimezuka tena katika Mji Mkuu wa Misri wakati vikosi vya usalama vinajaribu kuwaondoa waandamanaji kutoka medani ya Tahrir mjini Cairo.
Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi wakati waandamanaji waliokuwa katika medani hiyo wakivurumisha mawe na mabomu ya kujiundia ya moto.Hatahivyo maafisa wa chumba cha kuhifadhia maiti baadae leo wamesema kuwa idadi ya waliokufa hadi sasa ni watu wasiopungua 33.
Waziri wa utamaduni Emad Abu Ghazi amejiuzulu kutokana na ghasia hizo.
Mena-shirika rasmi la habari nchini humo limesema kuwa Waziri huyo amejiuzulu akipinga njia iliyotumiwa na serikali katika kukabiliana na waandamanaji.
Maandamanao haya ndiyo yamechukuwa muda mrefu zaidi tangu yale ya kumpinga Rais Hosni Mubarak mwezi February.
Waandamanaji wanahofu kuwa jeshi huenda linataka kung'ang'ania madaraka.
Baraza hilo, linaloongozwa na Field Marshal Mohamed Tantawi, linajukumu la kusimamia nchi hiyo wakati inaingia katika demokrasia baada ya miongo mitatu ya utawala wa kimabavu chini ya Bw. Mubarak.
Waandamanaji walisikika wakimtaka ajiuzulu katika maandamano hayo ya mwishoni mwa wiki.
"Wanajeshi waliahidi wataachia madaraka katika kipindi cha miezi sita" mmoja wa waandamanaji hao alisema."sasa miezi kumi tayari imeshapita na bado hawajatimiza ahadi zao, tunaona kama wanatuhadaa"