Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula amekuwa
mtu wa kwanza kujisajili Kanda ya Ziwa kushiriki mbio za Rock City Marathon,
huku akiwataka viongozi kuhakikisha wanafufua mchezo huo ili kuurejesha kwenye
hadhi yake kimataifa.
Akizindua usajili wa ushiriki wa mbio hizo jijini
hapa jana, Mabula alisema mbio hizo zinalenga kutambua na kukuza vipaji vya
riadha nchini, kutangaza vyanzo vya utalii na kuongeza kipato kwa vijana
ikizingatiwa kuwa michezo ni mojawapo wa fursa za ajira.
“Mnajua jinsi tunavyohangaika kutangaza utalii
wetu, lakini kupitia mashindano haya ambayo yapo kwenye kalenda ya mwaka ya
Chama cha Riadha Tanzania (RT) tutatangaza utalii wetu kupitia mchezo huu,”
alisema Mabula na kuongeza:
“Viwango vya riadha kwa miaka mitano tangu
mashindano haya yaanzishwe vimekuwa vikipanda, ambayo pia ni faida kwa
wadhamini ambao wanawekeza rasilimali watu na fedha, hivyo yamekuwa na
mafanikio.”
Alisema angependa mshindi wa kwanza hadi watatu
atoke jijini Mwanza ili kuendelea kutoa sifa kwa mkoa huu, lakini kubwa ni
fursa ya vijana kujipatia kipato kwa sababu hivi sasa michezo ni biashara.
Mabula aliwapongeza wadhamini wa Rock City
Marathon kwa mwaka huu kwa kusaidia kufanikisha uandaaji wa mashindano hayo kwa
mara nyingine tena katika jiji la Mwana, akiwataja kuwa ni Shirika la Hifadhi
ya Jamii (NSSF), Makampuni ya TSN kupitia kinywaji chake cha Chilly Willy
pamoja na African Barrick Gold, IPTL, Air Tanzania, New Mwanza Hotel, Nyanza
Bottling, Sahara Media Group, Continental decoders, New Africa Hotel, PPF, Tanapa
na Tanzania Tourist Board.
Waandaji wa mashindano hayo yanayotarajiwa
kufanyika Oktoba 26, Kampuni ya Capital Plus International Ltd (CPI) wamegawa
washiriki kwa madaraja mbalimbali; Mashindano kwa wote itakuwa kilomita 21,
kilomita tano ni kwa ajili ya walemavu wa ngozi (Albino) pamoja na washiriki
kutoka makampuni na mashirika mbali mbali, Wazee kuanzia umri wa miaka 55
watakimbia kilomita tatu na watoto chini ya umri wa 12 kilomita mbili.
Naye Kaimu Meneja wa Shirika la Hifadhi ya Jamii
(NSSF) Mkoa wa Mwanza, Shaaban Luanda ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano
hayo alisema Kazi yao kuu ni kuhifadhi jamii, hivyo kupitia michezo wanaamini
watakuwa wamelinda afya ya jamii.
Awali, akimkaribisha Mabula, Makamu Mwenyekiti wa chama
cha riadha mkoa wa Mwanza, Charles Kimune alisema licha ya changamoto
zinazokabili mashindano hayo kwa miaka mitano iliyopita, yamendelea kupata
mafanikio.
Mratibu wa mbio hizo, Mathew Kasonta alisema, “Wote
mnakaribishwa kuchukua fomu zinazopatikana katika ofisi za Capital Plus
International zilizopo posta mpya jengo la ATC ghorofa ya tatu, Chuo cha
Mtakatifu Agustino Mwanza, Ofisi zote za Utamaduni na Michezo wilaya ya Mwanza,
Uwanja wa Nyamagana na pia zinapatikana kwenye tovuti ya www.therockcitymarathon. blogspot.com
0 comments