Afrika
Kusini (Amajimbos) imewasili nchini kuikabili Tanzania (Serengeti Boys)
katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa
vijana wenye umri chini ya miaka 17 itakayochezwa keshokutwa (Julai 18
mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Timu
hiyo yenye msafara wa watu 37 ilitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) jana usiku (Julai 15 mwaka huu) na imefikia hoteli
ya Sapphire. Amajimbos itafanya mazoezi leo saa 10 jioni kwenye Uwanja
wa Azam Complex.
Waamuzi
watakaochezesha mechi hiyo kutoka Shelisheli wakiongozwa na Allister
Barra tayari wamewasili nchini. Kamishna wa mechi hiyo ni Andriamiasasoa
Doda Nirimboavonjy kutoka Madagascar.
Makocha
wa timu za Seregenti Boys na Amajimbos pamoja na manahodha wao watakuwa
na mkutano na waandishi wa habari kesho (Julai 17 mwaka huu) saa 5
asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kiingilio katika mechi hiyo ni sh. 2,000. Tiketi zitauzwa uwanjani katika magari maalumu siku ya mechi.
SAMATA, ULIMWENGU WATUA, MWINYI KAZIMOTO KESHO
Washambuliaji
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wamewasili nchini leo asubuhi (Julai
16 mwaka huu) kutoka Tunisia kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mechi
dhidi ya Msumbiji itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Wachezaji
hao wamefikia hoteli ya Courtyard, Seaview Upanga na leo (Julai 16
mwaka huu) watafanya mazoezi kwa programu maalumu waliyopewa na Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij wakati wakiwasubiri wenzao.
Naye
kiungo Mwinyi Kazimoto anayecheza mpira wa miguu katika klabu ya
Almarhiya ya Qatar atawasili nchini kesho (Julai 17 mwaka huu) saa 1.30
asubuhi kwa ndege ya Qatar Airways.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itawasili Dar es
Salaam kesho (Julai 17 mwaka huu) saa 3.20 asubuhi kwa ndege ya Fastjet
kutoka Mbeya tayari kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa Msumbiji.
RAIS MALINZI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa
na mkutano na waandishi wa habari Ijumaa (Julai 18 mwaka huu).
Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
0 comments