HERIETH PAUL, MWANAMITINDO WA KIMATAIFA AIPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA,ATEULIWA KUWA BALOZI WA KIMATAIFA WA KAMPUNI YA VIPODOZI YA MAYBELLINE – NEW YORK CITY

By Gadiola Emanuel - 1:42:00 AM


Herieth Paul mwanamitindo wa Kitanzania anayeishi jijini New York, Marekani ambako anafanyia kazi zake ameingia mkataba na kampuni ya vipodozi ya kimataifa ya MAYBELLINE ya New York, Marekani na kutangazwa kuwa BALOZI wake wa kimataifa  kuanzia mwezi Februari 2016; shughuli ambazo zitamfanya kwenda maeneo mbalimbali yakiwemo Bara la Ulaya, Marekani, Afrika, Asia na kwingineko duniani. Kampuni ya Maybelline ilimtangaza rasmi hivi karibuni, Mwanamitindo wa Kimataifa Herieth Paul, akiwa ni Mtanzania wa kwanza Mwanamitindo kuunyakua ushindi huu mkubwa.
 Herieth mwenye umri wa miaka 20 aligundulika kuwa na kipaji hicho akiwa na umri wa miaka kumi na nne (14) akiwa nchini Canada alipokuwa akisoma na kuishi na wazazi wake.

Mbali na uteuzi wa kuwa BALOZI wa kampuni ya Vipodozi ya Maybelline, Herieth Paul amefanikiwa kufanya kazi na makampuni mbalimbali ya mitindo na vipodozi duniani ikiwepo kampuni ya Diane Von Furstenberg, Lacoste, Tom Ford, Zac Posen, Phillip Lim, Mac, Sephora nk...,

Mwanamitindo wa Kimataifa Herieth Paul ambaye ameipeperusha Bendera ya Tanzania Dunia nzima anafanya masomo yake ya Chuo kwa njia ya mtandao na pia akijihusisha na shughuli za kijamii nyumbani alikozaliwa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwasaidia watoto yatima na wale wenye mazingira magumu  ili waweze kutimiza malengo yao ya kimaisha ikiwa ni pamoja na elimu na mahitaji yao ya kila siku.



Mafanikio ya Herieth ni mfano wa kuigwa na vijana wa Kitanzania kwa kuwa na uamuzi sahihi, malengo dhabiti na bidii ya kazi, ni vichocheo muhimu vinavyoweza kufanya mtu afanikiwe katika maisha.
Gazeti la GLAMOUR la New York, Marekani lilifanya mahojiano na Bi Herieth Paul wakati wa sherehe fupi ya kuteuliwa kwake iliyofanyika jijiji New York Marekani:

Lipstick:      Hongera kwa kuteuliwa kuwa Balozi wa Maybelline na kuwa mmoja kati ya wasichana waliokwisha kufanya kazi na kampuni hii. Je, kati ya wasichana waliowahi kufanya kazi na Maybelline ni nani anayekuhamasisha sana?.

Herieth:       Sijui niseme ni nani kati ya Christy Turlington na Jourdan Dunn. Christy ni mwanamke mwenye bidii ya kazi, ni mzazi na anasaidia mashirika yanayohudumia wasiojiweza. Jourdan pia ni mzazi na anatoa misaada kwa watu wengine.
                                
Lipstick:      Ni mwanamke gani anayekuvutia sana kwa urembo?

Herieth:       Mama yangu, ana uzuri wa asili, ngozi ya mwili ambayo ni nyeupe kidogo kuliko yangu ambayo inameremeta. Lakini pia anampenda Beyoncé.

Lipstick:      Katika kazi yako hii mpya kutakuwa na kila aina ya vipodozi. Kipodozi kipi unachokipenda zaidi?

Herieth:       Ninapenda kipodozi cha mdomoni chekundu na mara nyingi hujipaka kipodozi hiki ninapokuwa na marafiki zangu. Pia hupaka mascara kwenye kope na hasa hasa Maybelline “Falsies Puch Up Drama Mascara”. Hii naibeba kila mahali niendapo.

Lipstick:      Vipi, unapendelea mtindo gani wa nywele wakati wote?

Herieth:       Huwa nachana mitindo mbalimbali hasa napenda kuwa na nywele fupi. Natumia mafuta ya “Olive” yanayoitwa “Ecostlyer Gel”. Napaka nywele baada ya kuziosha asubuhi na kisha kuzifuta.  

Lipstick:      Hebu eleza ni wakati gani ulijiona umependeza na kwanini?

Herieth:       Hiki kinaonekana kama kitu cha mzaha lakini huu ndio muda wangu muafaka kueleza urembo wangu. Siku hiyo nilijipodoa mwenyewe. Niliweka nyusi za bandia, nikapaka rangi ya kahawia na rangi ya nude mdomoni. Nilipendeza na kuonekana mrembo sana. Kabla ya hapo niliangalia kwenye “Video ya Jaclyn Hill You Tube” namna ya kuremba “kope”. Akina mama wengi niliokutana nao walipendezwa na kuvutiwa na nilivyoremba “kope” zangu. Aidha waliniuliza nani aliyeniremba, niliwaambia nilijiremba mwenyewe.

Lipstick:      Vipi unaonaje kuhusu uchaguzi wa wasichana wa warembo kutangaza vipodozi na vifaa mbalimbali.

Herieth:       Mwaka 2011 nilipoanza kazi hii ya uanamitindo walikuwepo wasichana wachache sana weusi. Sasa hivi nawaona wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia kama vile bara la Asia, India n.k. Naona hali inaendelea kuwa nzuri, kuna mabadiliko na ninatumaini wasichana wengi wa aina hii wataingia katika kazi hii ya mitindo.

Lipstick:      Wakati wa sherehe ya mitindo ya mwezi, unatunzaje ngozi yako ya mwili wakati unatumia vipodozi vya aina nyingi bila kuiathiri ngozi yako?
Herieth:       Huwa nakwenda kwa mtaalamu wa utunzaji wa ngozi Mamie kila wiki. Yeye ndiye anahudumia wasichana wengi wenye ngozi nyeusi. Nahitaji mtu mwenye utaalamu wa ngozi yangu. Aidha huwa naangalia video kwenye mitandao ambayo inaniwezesha kutengeneza aina ya kipodozi ambacho ni rafiki kwa ngozi yangu. Pia nanunua aina mbalimbali ya vyakula ambavyo nachanganya na “distilled water” na “lavender oil” ambavyo natumia kila siku kurutubisha mwili wangu. Uzuri wa “hyaluronic acid” ni kuwa inaifanya ngozi yako ya mwili kuwa na unyevunyevu wakati wote. Naiweka kwenye jokofu wakati natumia, baada ya wiki naimwaga na kutengeneza nyingine. Ningependa kushauri wengine wanaopenda watumie pia wataona faida yake.

Lipstick:      Nini siri yako kuwa na nguvu wakati wote?

Herieth:       Ni mambo ya kawaida. Kwanza lazima nipate usingizi wa kutosha, lazima nilale kwa saa kumi (10). Naingia kitandani saa mbili (2) usiku. Marafiki zangu mara nyingine wananishangaa lakini nawaambia nisipopata usingizi wa kutosha asubuhi macho yangu yanakuwa mazito. Pia nafanya mazoezi ya viungo.


Lipstick:      Tumesikia kuwa unashughulika na misaada kwa watoto yatima. Hebu tueleze.

Herieth:       Nimejifunza na kuiga kutoka kwa mama. Tangu nikiwa mdogo nilikuwa namsikia na baadaye kuona mama anasaidia shule ya watoto yatima kule kwetu Tanzania. Mama amesaidia wasichana kadhaa ambao wengine wamemaliza masomo ya kidato cha sita (vi) na wengine wamekwenda kusomea kozi mbalimbali. Nami nasaidiana na mama kuwalipia karo vyuo vikuu, tunawanunulia vitabu, tunawapa pesa ya usafiri. Msaada huu utawasaidia katika maisha yao.

  • Share:

You Might Also Like

0 comments