Precision Air yazindua tovuti mpya na mitandao ya kijamii

By Gadiola Emanuel - 7:10:00 AM



Precision Air, shirika la ndege linaloongoza Tanzania leo imezindua tovuti yao mpya pamoja na kampeni maalum ya mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter ili kuweza kuimarisha uhusiano mzuri na kutoa huduma bora kwa wateja wao.  

Akizungumza kwa njia ya YouTube jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Biashara Bi. Lilian Massawe amesema kwamba tovuti hiyo mpya imetengenezwa mahususi kwa ajili ya wateja ili kuweza kuwapatia urahisi wa kupata taarifa mbali mbali za kampuni, na kukamilisha mipango yao ya kusafiri kwa ufanisi.

“Kati ya vitu vilivyoongezewa katika tovuti hii mpya ni taarifu muhimu kuhusu mtandao wetu wote wa sehemu 16 tunazosafiri, bila kusahau chombo maalumu ambayo mteja wetu anaweza kutumia kununulia tiketi yake ya safari akiwa sehemu yeyote duniani kupitia kadi za Visa na Master bila hata kufika ofisi za Precision Air kwa bei nafuu zaidi maana hata katwa makato ya huduma (service fee),” alisema Massawe.

Tovuti hiyo inayopatikana pitia www.precisionairtz.com pia inakuja na fomu ya malalamiko ya wateja ambayo itaruhusu kampuni kupata taarifa za moja kwa moja kutoka kwa wateja wao kokote waliko.

Wakati huo huo, shirika hili la ndege limezindua kampeni maalumu ya mitandao ya kijamii kupitia Facebook, Twitter na YouTube ili kuweza kwenda na soko la utandawazi wa kisasa wa njia ya mawasiliano kupitia intaneti utakaoweza kuwaongezea uwepo mkubwa zaidi kwa wateja wao.

“Kampeni yetu ya mitandao ya kijamii inalenga kuongeza uaminifu na ushirikishwaji wa moja kwa moja kwa wateja wetu. Pia tunaamini kwamba kupitia mitandao hii ya Twitter, Facebook na YouTube, kutakuuza idadi ya wateja kuwa wengi zaidi watakaotembelea tovuti yetu, pamoja na kutupa fursa ya kuwafahamu wateja wetu kwa undani zaidi,” alisema Afisa Mawasiliano wa Precision Air, Amani Nkurlu.

“Tunapenda kuwaalika washabiki wetu wote kutembelea mtandao wetu wa Facebook kupitia www.facebook.com/PrecisionAirTz na kutufuata katika Twitter kupitia www.twitter.com/PrecisionAirTz ili kuweza kuwasiliana nasi na kujishindia zawadi mbali mbali kutoka kwa Precision Air,” Nkurlu aliongeza.

Mwaka 2011 Precision Air ilizindua chombo maalum ya kukata tiketi kupitia mtandaoni yaani Internet Booking Engine yenye jina la Click and Fly kwa dhumuni la kurahisisha huduma ya ukataji tiketi kwa msafiri kupitia kadi za Master na Visa. Mwaka 2010 shirika pia ilizindua PW-SMS, bidhaa ambayo inamuwezesha msafiri kufahamu kuhusu mipango yake ya kusafiri kwa kupitia simu ya kiganjani tu.

Precision Air hivi sasa inasafiri kwenda miji mikuu yote ya Tanzania ikiwemo Mwanza, Bukoba, Musoma, Kigoma, Kilimanjaro, Arusha, Zanzibar, Mtwara na Dar es Salaam. Kikanda inasafiri kuelekea Nairobi na Mombasa nchini Kenya, Entebbe nchini Uganda, Hahaya nchini Comoros, Lubumbashi nchini Congo DRC, Lusaka nchini Zambia na Johannesburg nchini Afrika Kusini.

  • Share:

You Might Also Like

0 comments