MAJAMBAZI WA TANO WAKAMATWA

By Gadiola Emanuel - 2:16:00 AM

JESHI la Polisi Mkoani Arusha, linawashikilia majambazi sugu watano, wakihusishwa na matukio mbalimbali ya uporaji ikiwemo kuhusika katika tukio la uporaji wa pikipiki katika maeneo tofauti Mkoani Arushq.

Majambazi waliokamatwa wametajwa kuwa ni Peter Kavishe (32) mkazi wa Sanya Juu, Elimokozy Kavishe (29), Paulo Mallya (23) na Apolinari Mallya (21) wote wakazi wa Sanya juu na mwenzao Phillipo Semkondo (20) mkazi wa Unga limited Manispaa ya Arusha.

Akizungumzia tukio ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Thobias Andengenye, alisema kuwa, watuhumiwa hao wamekamatwa Mei 16 mwaka huu, majira ya saa 3.00 usiku huko eneo la France Kona mjini Arusha.

Alisema kuwa siku ya tukio dereva Abrahamu Eliamani ,mwenye pikipiki namba T.345 BGE aina ya Toyo, alikodiwa na Phillipo Semkondo ili ampeleke eneo la daraja mbili na alipofikishwa eneo hilo, ghafla alikabwa koo kwa nyuma na alipojaribu kusukumana na mtuhumiwa walitokea watu watatu na kumtisha kwa bastola na kisha kuondoka na pikipiki yake.

Kamanda Andengenye alisema kuwa baada ya kupora pikipiki hiyo Polisi walianza uchunguzi na ilipofika Julai mosi, walifanikiwa kumkamata Phillipo Semkondo, ambaye baada ya mahojiano alikiri na kubainisha kuwa,pikipiki hiyo imehifadhiwa eneo la Sanya Juu, mkoani Kilimanjaro.

Alisema kuwa baada ya polisi kufika eneo hilo walikuta idadi kubwa ya pikipiki zingine zikiwa zimehifadhiwa huko ambazo pia ziliporwa na watuhumiwa hao ambao waekuwa wakitumia eneo hilo kama chaka la kuhifadhi vitu vya wizi.

Andengenye alisema kuwa mtuhumiwa baada ya kubanwa aliwataja wenzake wengine watatu Elimokozy Kavishe, Paulo Mallya na Apolinari Mallya, ambao nao walikamatwa eneo hilo la Sanya Juu na wanashikiliwa kwa mahojiano na polisi.

Hata hivyo Polisi wameomba ushirikiano na Jeshi hilo, pale wanapofahamu mtu yoyote anajihusisha na matukio ya uhalifu na kutoa taarifa za siri, ili kukomesha matukio ya uporaji Mkoani hapa.

Washitakiwa hao watafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika, ili kujibu shitaka la wizi wa Pikipiki na tuhuma zingine.

  • Share:

You Might Also Like

0 comments